| Namba: 335625 | Tarehe: 2012/08/09 - 18:52 | Rejea: abna.ir | print |
Mkutano unaojadili maendeleo ya Syria kufanyika Iran |
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Ali Akbar Salehi, ameeleza kwamba nchi yake inajaribu kufufua baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa katika mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan. Salehi alieleza kwamba kati ya nchi 12 na 13 kutoka Asia, Afrika na Amerika ya Kusini zitashiriki katika mkutano huo lakini hakutaja ni nchi gani. Nchi chache zilizopelekewa mwaliko zimeshasema kwamba hazitaweza kutuma wawakilishi katika mkutano huo. Kuwait ambayo pia imetumiwa mwaliko, imekataa kushiriki, Lebanon imeeleza kwamba haitoweza kushiriki kwa sababu ya masharti ya sera ya uhusiano wake na Syria.
Naye waziri wa mambo ya nje wa Algeria, ametangaza kusikitika kushindwa kushiriki kwenye mkutano wa leo kwa sababu ya kuwa na shughuli nyingi. Hata hivyo atawakilishwa na naibu wake. Urusi imekubali pia kuuhudhuria mkutano wa leo utakaofanyika katika mji mkuu wa Iran, Tehran. Katika tamko lililotolewa hapo jana, wizara ya mambo ya nje ya Urusi, imesema kwamba nchi hiyo itawakilishwa na balozi wake wa Iran. Urusi imeahidi kuiwekea shinikizo Syria ili mapigano yanayoendelea nchini humo yaweze kusitishwa.